Wabunge nchini Sri Lanka Leo wanapiga kura itakayoamua nani atakuwa Rais wa Nchi hiyo ambapo Rais wa Mpito wa Nchi hiyo, Ranil Wickremesinghe ni miongoni mwa wagombea watatu wa Urais.

Usalama umeonekana kuimarishwa eneo la Bunge siku ya Jumatano asubuhi na duru za kisiasa zinasema kuwa endapo atachaguliwa Wickremesinghe maandamano makubwa yataendelea kwa kuwa Wananchi wengi hawamuungi mkono.

Wananchi wengi wameonekana kutomuunga mkono Wickremesinghe ambaye awali alihudumu kama Waziri Mkuu, na inahofiwa endapo atachaguliwa Maandamano zaidi yataendelea katika Taifa hilo lenye uhaba mkubwa wa Mafuta, Chakula na Dawa.

Mgombea mwingine ambaye anaungwa mkono na wananchi ni mtunga sheria wa chama Tawala Dullas Alahapperuma, ingawa hana nafasi ya juu serikalini na hana ushawishi katika serikali hiyo.

Mgombea wa tatu, Anura Kumara Dissanayaka, ambaye ni kiongozi wa watu wa Janatha Vimukti Peramuna anahitaji viti 3 katika Bunge hilo na hana uhakika wa kushinda.

Wickremesinghe alitangaza hali ya dharura akisema ilikuwa ni muhimu kwa maslahi ya usalama wa umma, kurejesha utulivu na huduma muhimu kwa maisha ya jamii wakati ambapo nchi inasubiri wabunge wapige kura.

Wabunge waliokutana siku ya Jumamosi walianza mchakato wa kumchagua kiongozi mpya kuliongoza taifa hilo.

Sri Lanka nchi ya kisiwa yenye wakaazi takribani milioni 22 hivi sasa ipo katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta.

Hadi kufikia siku ya Jumapili, vuguvugu la maandamano ilikuwa imefikia siku ya 100. Maandamano yamepungua kwa kiasi kikubwa tangu Rajapaksa aikimbie nchi na kujiuzulu, lakini baadhi ya watu karibu 500 wameendelea kukalia sehemu ya majengo ya Ikulu ya rais baada ya kuyavamia.

Aishi Manula mitatu tena Simba SC
Wagombea wenza 'watifuana' katika mdahalo