Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa wamepinga uteuzi wa wajumbe wa kamati 18 za Bunge uliofanywa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Wabunge hao wameeleza kuwa uteuzi huo umefanywa bila kuzingatia masuala muhimu. Viongozi wa Ukawa wamewataka wabunge wao kususia uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo.

“Tumeagiza wabunge wote wa Ukawa kutoshiriki kuchagua wenyeviti wa kamati hizi,” alisema John Mnyika ambaye ni naibu Katibu Mkuu wa Chadema.

Wabunge hao wameeleza kuwa uteuzi wa wabunge wa kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya umma (PAC na LAAC) ambazo kisheria zinatakiwa kuongozwa na mbunge wa upinzani, zimehujumiwa kwa kuwachagua wabunge wengi ambao ni wapya na wasio na uzoefu wa mambo mengi ya bunge, huku wenye uzoefu wakiangiwa kamati ambazo sio nyeti.

Ukawa wanaamini kuwa wenyeviti wa kamati hizo huchaguliwa kwa matakwa ya CCM kwa muda mrefu.

“Sisi tulitaka tupendekeze wabunge wa upinzani wanaopaswa kugombea uenyekiti katika kamati hizo mbili, si kupangiwa. Tumekuwa tukipangiwa muda mrefu na kubaini kuwa wenyeviti wa kamati hizo wanawekwa na CCM,” alisema Magdalena Sakaya.

Viongozi wa upinzani, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR – Mageuzi), Magdalena Sakaya (CUF), Tundu Lissu walifanya mkutano jana kujadili suala hilo.

Hata hivyo, katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila alisema kuwa hawajapokea malalamiko ya maandishi ya wapinzani hivyo wataendelea na utaratibu wa uchaguzi. Alisema kuwa wabunge wa CCM ni wengi katika kila kamati hivyo watatosha akidi na kufanya uchaguzi wao wenyewe kama wapinzani watasusia.

My Story: Alichonifanya huyu mrembo kwenye daladala kinaniuguza
Sababu Tatu Zilizomrejesha Mbwana Samatta DRC