Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, jana walisusia kushiriki mechi ya mpira wa miguu iliyoandaliwa kati ya wabunge na kati ya amani ya viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam wakimtaja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kama sababu.

Bunge liliandaa mechi hiyo mjini Dodoma ambapo vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinaendelea kwa lengo la kuwaleta pamoja wabunge na viongozi wa dini kama wadau wakuu wa amani nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wabunge wa Ukawa walisema kuwa walibaini kuna ajenda ya siri chini ya mechi hiyo kwakuwa hawakushirikishwa katika maandalizi hayo.

Aidha, Wabunge hao walidai kuwa walipata mualiko kutoka kwa Naibu Spika, Dk. Tulia ambaye bado wana tofuati naye na hawajamaliza mgogoro wao, huku wakidai kuwa viongozi hao wa dini walikuja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye alishindwa kuwatambulisha akiwa mkoani kwake.

“Timu iliyokuja kucheza nasi ilikuna na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye katika mkoa wake alishindwa kuwatambulisha kwa Rais, madiwani, mbunge na meya,” Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) amekaririwa.  “Ashughulike na matatizo yake ya Dar es Salaam,” aliongeza.

Naye Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema) alisema kuwa waliona kushiriki mechi hiyo kutaharibu mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kati yao na viongozi wa dini.

Kutokana na hali hiyo, viongozi hao wa dini walilazimika kucheza na maveterani huku mbunge mmoja pekee, Dk. Norman Sigalla wa Makete (CCM) akishiriki mechi hiyo.

Mechi hiyo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya wabunge tofauti na ilivyokuwa kwa mechi nyingine za wabunge zilizowahi kufanyika uwanjani hapo.

Picha: Majaliwa ashiriki Sala ya Iddi El Haji
Majaliwa aongoza Wananchi kuaga miili ya waliokufa tetemeko la ardhi, Atoa agizo TMA