Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametakiwa kufika mapema tarehe 16 Januari, 2022 mjini Dodoma ili kuanza vikao vya kamati za Bunge.
Wito huo umetolewa leo Tarehe 3 Januari na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Yustino Ndugai, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge jijini Dodoma.
“Niwaombe wabunge wote kufika mapema hapa Dodoma likizo zimeshaisha na sikukuu zimeisha, tarehe 16, Januari vikao vya kamati za Bunge vinaanza na Vikao vya Bunge vitaanza tarehe 1 Februari, 2022.” Alisema Spika Ndugai.
Aidha Spika Ndugai katika taarifa yake amesema tarehe 29, Januari wabunge wote watakuwa na hafla maalumu itakayoambatana na maombi kwa nchi na mgeni rasmi atakua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Tutakuwa na ‘National Prayer Breakfast’ tutafanya maombi ya pamoja ili kuliombea taifa na wananchi wote ili nchi iende salama,” aliongeza.
Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 1 Februari, unatarajiwa kuendelea kujadili taarifa mbalimbali na kuendelea kupitisha sheria kadhaa ili kuruhusu mkutano wa mwisho wa bajeti ambao unatarajiwa kuanza mwezi Aprili 2022