Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya, George Kinoti amewaita wabunge wanne kwa ajili ya kuwahoji kufuatia sakata la video ya ngono ambayo imekuwa ikihusishwa na Mbunge anayewakilisha wanawake, Fatuma Gedi bila uthibitisho.
Wabunge waliotajwa kwenye wito huo kwa mujibu wa Citizen, ni Aden Keynan wa jimbo la Eldas, Abdihakim Mohamed wa Jimbo la Fafi, Muwakilishi wa Wanawake wa Isiolo, Rehema Jaldesa na mwenzake wa Kirinyaga, Wangui Ngirici.
Wabunge hao wanatuhumiwa kumdhalilisha Gedi kwa kutoa matamko ambayo yanalenga kumchafua yakihusiana na video hiyo ya ngono.
Mwaka jana, mmiliki wa tovuti moja nchini humo alikamatwa na kuhojiwa katika Makao Makuu ya Ofisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuhusu video hiyo ambayo Mbunge Gedi amekana mara kadhaa kuwa mhusika.
Wabunge hao wanne pia wanatarajiwa kufika wiki hii kwenye Ofisi hizo kwa ajili ya kuhojiwa, ili sheria ifuate mkondo wake.