Baada yakuwasili jijini Dar es salaam ikitokea mkoani Kagera, ilikocheza mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC imejizatiti kuibuka na ushindi dhidi ya KMC FC kesho Jumamosi (Mei 07).
Azam FC itakua mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Azam Complex, huku ikikumbuka kisago cha bao moja kwa sifuri kutoka kwa Kagera Sugar Jumanne (Mei 03), katika Uwanja wa Kaitaba.
Uongozi wa klabu hiyo umekamilisha mpango wa kuwaweka sawa wachezaji kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya KMC FC, kwa dhamira ya kupata alama tatu muhimu na sio kuwania nafasi kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amesema: “Kujipanga ndio tumeanza kujipanga sasa, lakini kuweza kuishinda Presha, sio kazi ya uwanja wa mazoezi, ni suala la Kisaikolojia zaidi, na ndio kazi inayofanywa sasa.”
“Wachezaji wametakiwa kuuchukulia mchezo huo kwamba wanacheza na KMC FC, sio wanacheza na nafasi ya tatu au wanacheza na nani, waiangalie kama KMC FC na mchezo uwe huo huo, wakiweka mchezo mwingine kichwani wa kutaka kuingia Tatu Bora katika msimamo, watajipa mzigo mkubwa sana.”
“Wameambiwa Kila kitu kinawezekana kwa kushinda mchezo ulio mbele yao, wasiiwazie michezo ijayo, wasiwazie kitu ambacho watakipata baada ya kushinda, hicho ndicho wametakiwa kukifanya.”
Azam FC imeshacheza michezo 21 ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22 ikiwa nafasi ya nne kwa kufikisha alama 29. Ikishinda michezo minane, ikitoka sare michezo mitano na kupoteza michezo minane.