Nahodha wa kikosi cha Biashara United Mara Abul-Majid Mangalo ameushukuru Uongozi wa klabu hiyo kwa kufanikiwa ujio wa Kocha Mkuu mpya Khalid Adam.
Biashara United Mara ilitangaza kuachana na Kocha kutoka nchini Burundi Vivier Bahati na maafisa wengine wa Benchi la Ufundi mwanzoni mwa juma hili, kufuatia mwenendo wa timu hiyo kutoridhisha.
Mangalo amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake na kusema, Uongozi wao umefanya jambo muhimu la kumleta kocha huyo mzawa kwa haraka, na wao kama wapambanaji Uwanjani watahakikisha wanampa ushirikiano ili kufikia lengo la kubaki Ligi Kuu msimu huu.
Mangalo anayecheza nafasi ya Ulinzi, pia amewataka wadau wa soka Mkoani Mara kushikamana kwa pamoja ili kutoa motisha kwa wachezaji wa Biashara United Mara katika kipindi hiki, ambacho wanahitaji kufanikisha lengo la kupata alama tatu za kila mchezo.
“Tunashukuru Mungu Kocha Adam amefika kwa wakati, Uongozi umefanya jambo kubwa sana katika maamuzi haya, kilichobaki sisi wachezaji ni kumsikiliza na kupambana kwa ajili ya timu.”
“Tunafahamu kuna mtihani mkubwa sana mbele yetu, lakini tunaendelea kuhimizana kupambana kwa nguvu zetu zote ili kupata ushndi katika michezo iliyosalia na tuweze kufikia lengo la kubaki Ligi Kuu.”
“Wadau wa soka mkoani Mara tunawaomba waungane kwa pamoja, watambue umuhimu wa kuwa na hii timu katika kipindi hiki, ninaamini kama itakua hivyo hadi mwishoni mwa msimu, kila kitu kitakua safi na kila mmoja atafurahi.” Amesema Mangalo
Biashara United Mara hadi sasa ina michezo minne dhidi ya Kagera Sugar (Ugenini), Geita Gold (Ugenini), KMC FC (Nyumbani) na Azam FC (Ugenini).
Hadi sasa Biashara United Mara ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa alama 24, baada ya michezo 26.