Wachezaji wa Chelsea, wamekubali kukatwa asimilia 10 ya mishahara yao katika kipindi hiki cha janga la virusi vya Corona.
Nyota hao wamefanya majadiliano na kukubaliana kupitia kundi lao la mtandao wa kijamii wa WhatsApp, wakiongozwa na nahodha, Cesar Azpilicueta.
Jarida la Sportsmail, mwishoni mwa juma lililopita, liliripoti kwamba wachezaji wa Chelsea walikuwa wanajadiliana namna ya kukatwa mishahara na tayari wamefikia muafaka, ingawa bado haijathibitishwa na uongozi wa juu wa klabu kupitia kwa Mkurugenzi mtendaji, Marina Granovskaia.
Wakati huo huo umoja wa wachezaji wa ligi kuu England (Players Together), wameripotiwa kukusanya pauni milioni 4 kwa ajili ya kuchangia huduma za afya katika kipindi hiki cha kupambana na virusi vya Corona.
Fedha hizo zitawasaidia wahudumu wa afya walio mstari wa mbele kupambana na virusi vya Corona na maeneo mengine yenye uhitaji makubwa.