Uongozi wa FC Barcelona umekumbana na kikwazo kutoka kwa mastaa wao baada ya kugoma kukatwa mishahara ili kupunguza bili ya mishahara ipatikane pesa ya kumrudisha supastaa Lionel Messi huko Nou Camp.
Miamba hiyo ya La Liga ina matumaini makubwa ya kumrudisha Messi Nou Camp mara tu mkataba wake utakapofika tamati mwisho wa msimu huko Paris Saint-Germain.
Lakini, kwa Barca kumudu gharama za kumrudisha Messi kwenye kikosi chao, wanahitaji kupunguza bili yao ya mishahara kwa kiwango cha Pauni 180 milioni.
Kwa kufanya hivyo, Barca itakuwa na uwezo wa kufanya usajili wa mastaa wengine kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Katika kipindi cha miaka ya karibuni, wachezaji wa FC Barcelona wamekuwa wakikubali kukatwa mishahara yao ili kuisaidia klabu kifedha.
Lakini, kwa mujibu wa Sport, Franck Kessie na Andreas Christensen Wanaripoti wa kugoma kukatwa mishahara yao kwa kipindi hiki wakati klabu hiyo ikisaka unafuu kwenye bili yao ya mishahara ili imsajili Messi. Mastaa hao wawili wote walisajiliwa bure kutoka AC Milan na Chelsea.
Na sasa Barca watalazimika kutumia njia nyingine ya kupunguza matumizi ya kwenye klabu ili kuweza kutimiza ndoto yao.
Messi hivi karibuni alichochea matumaini ya kurudi Barca baada ya kuonekana akiwa na Sergio Busquets na Jordi Alba.