Katika kuhakikisha wanakua makini katika kujiandaa na mpambano wa mkondo wa kwanza wa mzunguuko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC, uongozi wa FC Platnum umeripotiwa kuzuia matuizi ya simu kwa wachezaji wa klabu hiyo.
Uongozi wa FC Platinum umetoa agizo hilo, baada ya kuzungumza na Kocha Mkuu Norman Mapeza, ambaye amedhamiria kuona kila mmoja kikosini kwake anakua makini na maandalizi ya mchezo dhidi ya Simba SC.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa, msukumo mkubwa wa agizo hilo kwa wachezaji umetoka kwa kocha Mapeza, ambaye aliamua kulipitishia kwa viongozi ambao muda wote wameonekana kuwa kwenye umakini mkubwa.
Kitendo cha Simba kuwasili mapema mjini Harare, kimetajwa kama chanzo cha kocha wa FC Platinum, kuzuia matumizi ya simu kwa wachezaji wake, ambao walizoea kufanya hivyo chini ya kocha ambaye alifukuzwa kabla ya kuanza michuano ya kimataifa.
Mchezo wa mkondo wa kwanza kati ya wawili hao utachezwa kesho Jumatano (Desemba 23) kwenye Uwanja wa Taifa mjini Harare, Zimbabwe kabla ya mchezo wa mkondo wa pili kupigwa jijini Dar es salaam kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa mwanzoni mwa mwezi Januari 2021.