Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Nassor Hamduni, amekemea tabia ya baadhi ya wachezaji kuwazingira, kuwakemea na kuwatisha waamuzi Uwanjani, hasa wa kike

Hamduni ambaye ni mwamuzi wa zamani wa kimataifa, amesema kuwa baadhi ya wachezaji wameonekana kuwa na utovu wa nidhamu kwa waamuzi, hasa wa kike, kwa kupinga uamuzi wao na kuonekana kuwatolea maneno yasiyofaa.

“Hii si vizuri hata kidogo! Na kwa sababu inaonekana kwenye televisheni, wengine wakiona wanaendelea na tabia hii.

“Ninawapongeza sana waamuzi wetu kwa sababu nao hawaingii kwenye jazba ya wachezaji badala yake wanafuata sheria na kanuni inavyomwelekeza, vinginevyo kama na wao wangekuwa wanajibu mapigo, na wao ndiyo wanaoamua kila kitu uwanjani, sidhani kama hali ingekuwa nzuri,” ameonya.

Amesema ameona baadhi ya mechi wachezaji wakiwazonga waamuzi wa kike, akitoa mfano mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Singida Fountaine Gate dhidi ya Simba SC aliona baadhi ya wachezaji walikUwa wanamsumbua mwamuzi Amina Kyando.

“Waamuzi wetu wanatumia busara sana kwa sababu nchi zingine huwezi kumzonga, kumshika, wala kumzunguka mwamuzi ukimfokea. Hili jambo mimi ninaomba wale wachezaji wenye tabia hiyo waache kwa sababu yeye akishatoa uamuzi, hata ufanye nini hawezi kubadilisha,” alisisitiza.

Hamduni amesema wachezaji wa sasa wanapata bahati ya kuchezeshwa na waamuzi vijana, hivyo wawe na nidhamu na upendo kwao kwa kuwa zamani wachezaji wengi walikuwa wakichezeshwa na waamuzi wenye umri mkubwa sawa na baba zao.

NEC yatoa vibali elimu ya mpiga kura uchaguzi mdogo
Balozi Yacoub wasilisha hati za utambulisho UAE