Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed ‘Mo’ Dewji, imeahidi kutoa kiasi cha Shilingi milioni 400 za Kitanzania kwa wachezaji na benchi la ufundi baada ya kukunwa na kipigo dhidi ya watani zao, Young Africans.
Chanzo chetu ndani ya klabu hiyo kimetueleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed ‘Mo’ imefurahishwa na ushindi huo na wameafiki kutoa zawadi ya kiasi hicho cha pesa.
Simba SC waliibanjua Young Africans mabao manne kwa moja katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) juzi Jumapili.
Mabao ya Simba katika mchezo huo uliounguruma uwanja wa Taifa Dar es salaam yalifungwa na Gerson Fraga, Clatous Chama, Luis Miquissone na Muzamiru Yassin.
Ushindi huo unaipelekea Simba SC Fainali ya ASFC, mchezo utakaounguruma mjini Sumbawanga mkoani Rukwa mwanzoni mwa mwezi ujao.
Simba SC watacheza dhidi ya Namungo FC ambao walikata tiketi ya kucheza Fainali siku ya jumamosi, baada ya kuicharaza Sahare All Stars bao moja kwa sifuri, Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.