Kocha Mkuu wa Simba SC Robert Oliveira ‘Robertinho’ amesema ameanza kazi ya kuivutia kasi Wydad Casablanca ya Morocco atakayokutana nayo katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, lakini amewataka wachezaji kuacha kuwafikiria kwa kuwa bado wana mchezo mgumu dhidi Ihefu FC na Young Africans.
Simba SC itasafiri hadi mjini Mbarani mkoani Mbeya keshokutwa Jumatatu (April 10) kwa ajili ya kucheza dhidi ya Ihefu FC itakayokuwa nyumbani Highland Estate, kisha itarejea jijini Dar es salaam kujiwinda na mchezo dhidi ya Young Africans utakaopigwa April 16 na baada ya hapo shughuli dhidi ya Wydad Casablanca itaanza rasmi.
Kocha Robertinho amesema tayari amewafuatilia wapinzani hao kutokanchini Morocco katika mchezo wa Dabi dhidi ya Raja Casablanca na ataendelea kufanya hivyo ili kuandaa mikakati yake ya kuhakikisha wanashinda katika mchezo wa Robo Fainali na kutinga Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Amesema wakati akifanya hivyo kwa kushirikiana na Benchi lake la Ufundi, Wachezaji wake kwa sasa hawapaswi kuweka nguvu kubwa ya presha katika mchezo wao Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa bado wana michezo muhimu ya ligi Kuu ikiwemo dhidi ya Young Africans.
“Kitu ambacho tulikuwa tunakisubiria ni kujua tutakutana na timu gani katika hatua ya Robo Fainali lakini siyo kuweka nguvu kubwa huko tukiwa bado tuna michezo mingine migumu katika Ligi Kuu Bara, tunatakiwa kucheza dhidi ya Ihefu kwenye ligi halafu Young Africans michezo ambayo yote matokeo kwetu ni muhimu.”
“Kila mchezaji anatambua kuwa malengo yetu yapo kutoka mchezo mmoja kwenda mwingine kwa sababu tumeshajua nani tutacheza naye lazima tuweke nguvu kubwa kwenye hii michezo ya ndani kwa sababu ukiangalia mchezo dhidi ya Young Africans ambao wanaongoza ligi hautokuwa wa kawaida kutokana upinzani wa jadi uliopo kati yetu,”
“Binafsi kwa kushirikiana na wenzangu katika Benchi la Ufundi tumeshaanza kazi ya kufuatilia kwa ukaribu ubora na udhaifu wa Wydad Casablanca, tumefanya hivyo katika mchezo wao wa ligi dhidi ya Raja Casablanca na tutaendelea kufanya hivyo ili kutengeneza mpango wa maandalizi, lakini hii ni kwetu sisi Benchi la Ufundi wachezaji wanapaswa kuendelea kufikiria kilichopo mbele kwa sasa, hasa michezo ya ndani.” amesema Robertinho.
Jana Ijumaa (April 07) Simba SC ilicheza mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Ihefu FC, ambayo imekubali kutupwa nje ya michuano hiyo kwa kukubali kichapo cha mabao 5-1.