Baada ya kurejea kutoka Jijini Mwanza walikocheza mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Young Africans, wachezaji wa Simba SC wamepewa mapumziko ya majuma mawili.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC Ahmed Ally amesema Benchi la Ufundi chini Kocha Mkuu Pablo Franco lilitoa mapumziko hayo, ili kuwapa muda wachezaji wa kurudi katika familia zao na kufanya mambo yao binafsi.
Ahmed Ally amesema baada ya majuma mawili, wachezaji wa Simba SC watarejea kambini kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu iliyosalia msimu huu 2021/22.
“Baada ya kurudi kutoka Mwanza wachezaji ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa walipewa mapumziko ya majuma mawili, benchi la ufundi limeona kuna haja ya wachezaji kuwa mapumzikoni katika kipindi hiki ambacho timu za taufa zinajiandaa na michezo wa kuwania kufuzu AFCON 2023.”
“Watakaporejea wachezaji wetu watakua na kazi ya kuhakikisha wanapambana na kushinda michezo iliyobaki katika Ligi Kuu ili kukamilisha msimu kwa kupata alama 3 za kila mchezo.” amesema Ahmed Ally
Katika hatua nyingine Ahmed Ally amesema Klabu hiyo itafanya Usajili Mkubwa kwenye Dirisha lijalo la Usajili huku wachezaji kadhaa wakitarajiwa kuachwa.