Kiungo wa Simba SC Clatous Chotta Chama pamoja na baadhi ya mastaa wa Young Africans wameweka wazi mipango na matarajio ya timu zao kuelekea Robo Fainali ya Michuano ya Klabu Barani Afrika.

Simba SC imepangwa kukutana na Mabingwa Watetezi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Wydad Casablanca ya Morocco, huku Young Africans ikiangukia mbele ya Mabingwa wa Soka wa Nigeria Rivers United katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Clatous Chama amesema; “Tunatambua ubora wa Wydad, ni timu ngumu na yenye uzoefu wa kutosha na mashindano haya wakiwa mabingwa watetezi lakini hilo halituzuii kufanya vizuri.”

“Simba SC tuna timu nzuri pia tunataka kuvuka hatua hii na kufika nusu fainali hivyo kama wachezaji, tupo tayari kwa mapambano na kuhakikisha tunafuzu Nusu Fainali.”

Kwa upande wa Nahodha msaidizi na Beki wa Young Africans, Dickson Job, amesema kufika Robo Fainali Kombe la Shirikisho lilikuwa lengo la kwanza kwa klabu yao na sasa wanatambua umuhimu wa kupata matokeo ya ushindi ili waweze kufika hatua nyingine na wanawaheshimu wapinzani wao hivyo wataingia kwa tahadhari.

“Tunakutana na timu ambayo tayari tumepata nafasi ya kucheza nayo na matokeo dhidi yao hayakuwa mazuri hivyo hatuwezi kufanya makosa kwa kurudia kile kilichotokea,”

“Ni timu nzuri lakini na sisi ni bora hivyo dakika 90 zitaamua ubora wetu na wao malengo yetu kama timu ni kuvuka hatua ya Robo na kuingia Nusu Fainali.”

Kwa upande wa Farid Mussa na Jesus Moloko wamesema wanatambua wamefikia hatua ngumu ya mtoano na wanatakiwa kushindana ili wasonge mbele.

Farid Mussa amesema wao kama wachezaji lengo lao ni moja watapambana kuhakikisha wanapata alama zote sita nyumbani na ugenini na kujitengenezea nafasi ya kusonga hatua inayofuta huku akikiri hilo linawezekana wakiwekeza nguvu kwa pamoja.

Simba SC itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuikabili Wydad Casablanca kati ya April 21-22, kisha itakwenda mjini Casablanca kwa mchezo wa mkondo wa pili ambao umepangwa kupigwa kati ya April 28-29.

Young Africans itaanzia ugenini Aprili 23, mwaka huu katika Uwanja wa Adokiye Amiesimaka uliopo katika Port Horcout, Rivers nchini Nigeria, huku mchezo wa pili ukipangwa kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam April 30.

Kazi kubwa Ligi Kuu ya England
Mwakinyo apata sapoti, Milioni 35