Kiungo kutoka nchini Brazil Bruno Gomes na Beki kutoka DR Congo Biemes Carno wamesema kikosi cha SIngida Big Stars hakitacheza kinyonge dhidi ya Young Africans katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho Alhamis (Mei 04) Uwanja wa CCM Liti mkoani Singida.
Singida Big Stars itaikaribisha Young Africans katika mchezo huo, kisha itakuwa tena mwenyeji dhidi wa wababe hao wa Jangwani katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Bruno amesema wanaiheshimu Young Africans lakini safari hii hawapo tayari kuona tena wanapoteza kizembe kama ilivyokuwa mchezo wa kwanza waliofungwa mabao 4-1, Novemba 17 mwaka jana, katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.
“Kila mmoja wetu anatambua ubora wa Young Africans msimu huu ila sisi kama wachezaji tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ambayo nasi yatakuwa na manufaa makubwa wakati tukibakiwa na michezo michache,” amesema.
Kwa upande wa beki wa kati wa timu hiyo, Carno Biemes amesema michezo yao miwili mfululizo na Young Africans inakuja katika wakati mzuri kwani itatoa taswira nzima kwao ya kuweza kupata taji lolote na kumaliza nafasi ya tatu.
“Kwenye ligi kwa sasa tunapigania nafasi tatu za juu na ukiangalia sisi na Azam FC ndio washindani, sasa ili kujiwekea mazingira mazuri ni lazima katika kila michezo yote iliyobaki tuna hakikisha tunafanya vizuri.”
Carno amesema licha ya hayo ila pia wana nafasi ya kumaliza msimu na Kombe la ASFC hivyo jitihada kubwa kwao kama wachezaji wamewekeza huko ingawa siyo rahisi kutokana na ushindani uliopo miongoni mwa timu zilizopo.