Meneja wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino, amewashutumu wachezaji wake kwa kushindwa kuonyesha nidhamu ya mchezo, pindi walipokutana na Olympiakos usiku wa kuamkia leo.
Mchezo huo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, ulishuhudia miamba hiyo ikitoka sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili.
Pochettino amesema kilichotokea ni uzembe wa hali ya juu kwa wachezaji wake, ambao muda wote walipaswa kucheza kwa nidhamu, lakini suala hilo halikuonekana kikamilifu wakati wote.
Amesema anaamini walikua na sababu kubwa ya kushinda ugenini, na walionyesha hivyo kipindi cha kwanza walipokua wakiongoza mabao mawili, ila hatua ya kubweteka kwa wachezaji wake ilikua kichocheo kikubwa kwa wapinzani wao kurejea mchezoni na kusawazisha.
“Sikuona sababu zozote za wapinzani wetu kupewa nafasi ya kucheza kwa kujiamini kiasi kile, tuliwadharau kwa kuamini tumeshashinda mchezo, nimesikitishwa sana na hali hii,”
“Kiujumla nidhamu ya mchezo kwa wachezaji wangu ilishuka maradufu baada ya kuongoza mabao mawili, sitegemei kama jambo hilo litajirudia tena katika michezo inayofuata.” Alisema Pochettino
Spurs waliokua ugenini, walianza kupata bao la kuongoza dakika ya 30 kwa mkwaju wa penati iliyopigwa na Harry Kane, na baadae Lucas Moura alifunga bao maridadi na kuiwezesha klabu hiyo ya jijini London kuongoza mabao mawili kwa sifuri.
Dakika chache kabla ya mapumziko wenyeji Olympiakos, walipata bao la kwanza kupitia kwa Daniel Podence, kabla ya Mathieu Valbuena hajafunga la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 54.
Mchezo ujao Spurs watakua nyumbani jijini London wakiwakaribisha mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich, ambao jana walianza vyema hatua ya makundi kwa kupata ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya FK Crvena Zvezda ya Serbia.