Wakati Bodi ya Ligi ikipendekeza ligi iendelee wiki ya kwanza ya mwezi Juni bila mashabiki, kiongozi wa wachezaji wa Young Africans, Papy Kabamba Tshishimbi amesema wiki mbili tu zinawatosha kujiweka sawa kukinukisha.
Bodi ya Ligi imependekeza ligi kuendelea wiki ya kwanza ya Juni katika kikao kilichofanyika mara baada ya kauli ya Rais John Pombe Magufuli kueleza kuwa anafikiri ligi iendelee lakini atashauriana na wataalamu.
Tshishimbi alisema kwa kuwa wachezaji wa Yanga wanafanya mazoezi binafsi huko majumbani chini ya uangalizi wa makocha, haitakuwa tatizo kwao kuanza ligi kama ambavyo Bodi inapendekeza kama Serikali itaruhusu.
“Tutahitaji wiki mbili kufanya mazoezi ya pamoja tu, kipindi hicho kinatosha kabisa, kwani hivi sasa tunajifua binafsi, haitakuwa tatizo,” alisema mchezaji huyo huku akiongeza hata wenzake wanaafikiana na hilo na wamekuwa wakiwasiliana kwa njia mbalimbali hasa kwenye WhatsApp.
Alisema kwamba ana uhakika huko waliko wanajifua kwelikweli kwavile huwa wanapeana mirejesho ya kila kinachofanyika.
Kocha wa Young Africans Luc Eymael ameunga mkono kurejea kwa ligi huku akisema kuanzia sasa amebadili program na wachezaji wake watakuwa wanapasha mara mbili kwa siku.
Aidha, wachezaji wengine wa klabu za Ligi Kuu wametoa maoni yao.
Mpachika mabao wa Namungo, Reliants Lusajo alisema kama watapewa wiki tatu au mbili za maandalizi ya pamoja kabla ya ligi kuendelea, itakuwa nafuu kwao.
Nahodha wa Azam FC, Agrey Morris ametofautiana na Lusajo akieleza kuwa mwezi mmoja ndiyo utafaa zaidi kufanya mazoezi ya pamoja.
Kipa wa KMC na Taifa Stars, Juma Kaseja alisema kwa mchezaji ambaye anafanya mazoezi binafsi muda wowote ligi itakapoendelea haitokuwa tatizo kwake kama ilivyo kwake.