Meneja wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho ana matumaini ya kuwatumia wachezaji wote waliokua katika vikosi vya timu za taifa zilizofika hatua ya mwisho ya fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwezi uliopita, wakati wa mchezo wa ufunguzi wa ligi ya England dhidi ya Leicester City siku ya Ijumaa.
Mourinho amekua katika mashaka ya kuwatumia wachezaji hao kutokana na kuwa katika likizo ya mapumziko ambayo iliingiliana na muda wa maandalizi ya msimu, hali ambayo ilikidhohofisha kikosi cha Mashetani Wekundi katika baadhi ya michezo ya kirafiki.
Tayari baadhi ya wachezaji waliokua katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi wameshajiunga na wenzao tangu juma lililopita na walikua sehemu ya kikosi cha Man Utd kilichoecheza mchezo wa mwisho wa kujipima nguvu dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich siku ya Jumapili.
Wachezjai hao ni Victor Lindelof (Sweden), Marcus Rashford na Phil Jones (England).
Mourinho amesema mshambuliaji Rashford tangu alipojiunga na kambi ya maandalizi ya kikosi chake amekua na maendeleo mazuri, na ana uhakika atakua fit kwa ajili ya mchezo wa Leicester City siku ya Ijumaa.
“Lindelof na Jones wote wameonyesha kuwa tayari kama ilivyo kwa Rashford, nina matarajio ya kuwatumia katika mchezo wetu wa kufungua msimu huu.” Alisema meneja huyo kutoka Ureno.
Wachezaji wengine ambao wanatarajiwa na Mourinho kuwa sehemu ya kikosi siku ya Ijumaa ni Ashley Young, Jesse Lingard, Marouane Fellaini, Paul Pogba na Romelu Lukaku.