Wachezaji wa klabu ya Arsenal wamemkingia kifua meneja wao Unai Emery, baada ya kuona anashambuliwa na baadhi ya wadau wa soka nchini England, kufuatia kuanza vibaya msimu huu kwa kufungwa na mabingwa watetezi wa ligi ya nchi hiyo Manchester City, mabao 2 – 0 mwishoni mwa juma lililopita.
Wachezaji wa Arsenal kwa pamoja wametuma ujumbe kwa wadau wa soka nchini England wakisema, meneja huyo anapaswa kuachwa na kuheshimiwa, hasa katika kipindi hiki ambacho ameanza kazi.
Wachezaji wamesema wanafurahishwa na uwepo wa meneja huyo kutoka nchini Hispania na suala la kupoteza mchezo dhidi ya Man City, ni la kawaida kutokana na mchezo wa soka kuwa na matokeo ya aina tatu, kufungwa, kushinda na kutoka sare.
Hata hivyo taarifa ya wachezaji wa Arsenal imewataka mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuwa na imani na timu yao, pamoja na kutokatishwa tamaa na maneno yanayoendelea dhidi ya Unai Emery ambaye amechukua mikoba ya babu Arsene Wenger.
Baadhi ya wadau wa soka nchini England wamekua wakiponda mfumo wa meneja huyo, kwa kusema hauwezi kutoa ushindani katika ligi ya England na ulikua chanzo cha kuruhusu kikosi chake kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Man City kwa kiufungwa mabao mawili kwa sifuri.
Arsenal inaendelea kujiandaa na mchezo wa mzunguuko wa pili wa ligi kuu ya England, utakaowakutanisha na mabingwa wa kombe la FA Chelsea FC, kwenye uwanja wa Stamford Bridge mwishoni mwa juma hili.