Wakati timu zingine zikitoa mapumziko ya siku kadhaa kwa wachezaji wake kutokana na mapumziko ya Kalenda ya FIFA, kikosi cha wachezaji wa Young Africans ambao hawakuitwa kwenye timu zao za taifa kitaendelea na mazoezi kama kawaida kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Oktoba 25.
Meneja wa klabu hiyo, Walter Harrison, amesema kuwa wachezaji wote wa timu hiyo ambao hawajachaguliwa kwenye vikosi vya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa wachezaji wazawa na timu za mataifa mengine wataendelea na ‘program’ ya mazoezi kama kawaida kwa sababu wana mchezo mgumu dhidi ya Azam FC.
“Tuna wachezaji 11 ambao wataondoka kwenda kuzitumikia klabu zao za taifa, kuna wachezaji wa Tanzania, Mali, Uganda, Burkina Faso, wataelekea kuziwakilisha nchi zao, lakini wale ambao hawajaitwa kwenye timu yoyote ya taifa watakuwa hapa hapa nchini kwa ajili ya ‘program’ za mazoezi kujiandaa na mchezo utakaofuata dhidi ya Azam FC Oktoba 25 kama hakutokuwa na mabadiliko ya ratiba, na mazoezi yataendelea hadi hapo waliokwenda kwenye timu za taifa watakaporejea, wataungana na wenzao hapo sasa tutakuwa tuna kikosi kamili kwa ajili ya mechi yetu inayofuata.” Amesema meneja
Wachezaji wa nje ambao wanatarajia kwenda kwenye vikosi vya timu ya taifa ni Khalid Aucho akienda kuichezea timu yake ya Uganda Cranes, Stephane Aziz Ki, akienda kulitumikia taifa lake la Burkina Faso na Djigui Diarra anayerejea kuidakia timu yake ya Taifa ya Mali, huku waliosalia ambao ni wazawa, watakwenda kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Tayari Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, ameshaanza kuifungia kazi Azam FC kwa kuangalia mikanda ya video ya timu hiyo ilivyocheza mechi zake za Ligi Kuu msimu huu ili kung’amua ubora na udhaifu wa timu hiyo, hivyo amesema anahitaji muda mrefu wa kuwa na wachezaji ili kuwatengeneza kuweza kudhibiti ubora wa wapinzani wao na kuutumia udhaifu wao kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mechi ijayo.
Young Africans inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa ikiwa na pointi 12 kwa mechi tano ilizocheza mpaka sasa, ikishinda mechi nne na kupoteza moja.