Maeneo mengi zinapofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi, yameanzishwa bila kufuata utaratibu, ikiwemo kutuma maombi kwa Mkurugenzi na kufanya ukaguzi au tathmini ya mazingira ili kuona iwapo kuna uwezekano wa kuwepo kwa athari za kimazingira ambapo pia Serikali imekuwa ikikosa mapato.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Katavi, Faustine Maijo amesema uchambuzi wa mifumo wa miezi mitatu iliyopita umebaini pia wamiliki wengi wa maeneo ya machimbo ya madini ujenzi, hawana leseni za biashara hiyo kama ambavyo Sheria ya Madini Na. 14/2010 kifungu cha 47 inavyoelekeza.
Maijo ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake hii leo Agosti 24, 2022, amesema maeneo mengi ya uchimbaji wa madini ujenzi mkoani humo sio rasmi na hayana vituo vya ukaguzi wa madini ujenzi, daftari la kuorodhesha magari yanayopita na mashine za kielektroniki (POS) kwa ajili ya kukusanya ushuru.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa TAKUKURU, amesema uchambuzi wa mfumo wa utendaji kazi kwa upande wa wakala wa huduma za ufundi umeme (TEMESA), umebainika kuwa gharama za vipuri ziko juu, mafundi wachache, magari kukaa muda mrefu wakati wa matengenezo ambayo pia yana gharama za juu na magari kupelekwa gereji ambazo sio za TEMESA, na kuisababishia Serikali kukosa mapato kutoka kwa wakala huyo.