Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa amewataka wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu wa mgodi wa Namungo kuzingatia Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali wanapokuwa wanatekeleza shughuli za uchimbaji.

Ameyasema hayo Kijijini Namungo wilayani Ruangwa wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Matumizi Salama ya Kemikali kwa wachimbaji hao yanayotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kusini.

“Nawaomba wachimbaji wa mgodi huu mtumie fursa hii ya mafunzo kujifunza Sheria zinazohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali ili muweze kuzingatia matumizi salama ya kemikali katika shughuli zenu kwa lengo la kulinda afya zenu na mazingira yanayo wazunguka, kwani natambua uchimbaji wa dhahabu unahusisha matumizi ya kemikali na hakuna kemikali isiyo na madhara duniani,”amesema Mgandilwa

Aidha, amesema kuwa sekta ya madini ni sekta muhimu sana katika uchumi na ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano inajitahidi kuwawekea mazingira mazuri wachimbaji ili kuhakikisha wanafaidika na kazi hizo pia wanalinda afya zao kwa kuwa athari za kemikali nyingine zinaweza kuonekana baada ya miaka mingi.

Kwa upande wake Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba, David Elias amesema kuwa Mamlaka hiyo imeamua kuwafikia wadau wake na kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya kemikali ili kuepusha madhara makubwa ya kiafya na kimazingira yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo salama ya kemikali.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya uchimbaji ya Gemini, Alfred Michael ameishukuru Mamlaka hiyo kwa kuamua kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika kuimarisha shughuli zao za uchimbaji hasa kwenye matumizi ya kemikali.

Hata hivyo, mafunzo hayo yamehusisha jumla ya wachimbaji wadogo wadogo 50 kutoka Kampuni za uchimbaji za Gemini na Majini zinazojihusisha na uchimbaji wa dhahabu kwenye mgodi wa Namungo uliopo wilayani Ruangwa katika Mkoa wa Lindi.

Wafungwa Kenya wataka kuongezwa mshahara
Chriss Brown amtaka Eddy Kenzo, Ghetto Kids wimbo wake mpya