Chama Cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Njombe (NJOREMA) kimetoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John pombe Magufuli kwa uzalendo na kila dhana aliyoiangazia kwa wachimbaji na Tasnia ya madini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa chama hicho na makamu wa Raisi wa shirikisho la vyama vya wachimba madini Tanzania (FEMATA) Alfred ambapo ameahidi kupeleka elimu kwa Wakazi wote wa Njombe kuhusu ulipaji wa kodi kwa hiari huku wakipinga utoroshaji wa madini kwa nguvu zote.
“Maudhui ya makutaniko haya ni kumshukuru Rais kwa upeo,upendo,umahiri na uzalendo na kila dhana njema aliyoielekeza kwetu wachimbaji kwani jambo hili sio raisi limethibitishwa kwake , jinsi kwa miaka mingi toka uhuru lilivyofumbiwa macho”amesema Luvanda
Baadhi ya wachimbaji wameiomba serikali kushirikiana kuwa saidia wachimbaji kupata leseni kwa wakati pamoja kupunguziwa baadhi ya maeneo makubwa yaliyoshikiliwa na mashirika pamoja na wachimbaji wakubwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe, Emmanuel George amesema kuwa kwa sasa wachimbaji wana wajibu wa kubadilika na kuto kufanya kazi mtu mmoja mmoja badala yake waungane ili kufanya kazi kibiashara na kuukuza mkoa wa Njombe kama ilivyo katika mazao mengine ikiwemo zao la chai.
Hata hivyo, chama hicho cha wachimbaji wa madini mkoa wa Njombe kimeungana na Vyama vingine nchini kutoa pongezi hizo kwa Rais kwa kuweza kuwatatulia changamoto mbalimbali katika uchimbaji wa madini.