Wizara ya mifugo na uvuvi, imesema itaendesha mafunzo kwa wachunaji ngozi katika machinjio ya mikoa yote ta Tanzania Bara ili kuhakikisha mnyoro mzima wa mazao ya mifugo ikiwemo ngozi inakuwa na thamani inayoviwezesha viwanda vya kutengeneza ngozi kupata malighafi yenye ubora inayozalishwa nchini na ziada kuuzwa nje ya nchi.
Baada ya ukamilishaji wa mafunzo hayo, wizara imesema itachukua hatua ya kufungia machinjio ambazo zitakosa kuwa na wachunangozi waliorasimishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za wizara ya mifugo na uvuvi.
Hayo yamebainishwa na naibu waziri wa Mifugo na uvuvi, Abdalah Ulenga wakati akikabidhi leseni za wachunangozi 161 waliorasimishwa wa manispaa ya Morogoro waliohitimu mafunzo ya namna bora ya kuchuna na kuhifadhi ngozi wenye vigezo vilivyowekwa.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha mnyororo mzima wa mazao ya mifugo ikiwemo ngozi inakuwa na thamani inayo viwezesha viwanda vya kutengeneza ngozi kupata malighafi yenye ubora inayozalishwa hapa nchini.
Ulenga amesema licha ya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa idadi ya mifugo kwatika bara ya Afrika lakini wastani wa asilimia 50 ya ngozi inaharibika kwenye uchunaji na kupoteza ubora na uhafifu wa ngozi hivyo kusababisha baadhi ya weneye viwanda kulazimika kuingiza ngozi kutoka nje ya nchi.