Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara amewaonya Walimu, Wazazi na Wanafunzi kutoshiriki vitendo vya wizi, ununuaji au udanganyifu wa mitihani ya kidato cha nne iliyoanza leo Novemba 4, 2019 nchini kote.
Waitara ametoa onyo hilo Jijini Dodoma wakati akitoa salamu za heri kwa wanafunzi zaidi ya Laki nne, na kusema watakaojaribu kukiuka agizo hilo wataangukia katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua.
Amesema kumekuwepo na vitendo vya udanganyifu wakati wa vipindi vya mitihani ya Kitaifa na kuwataka wazazi na wanafunzi kutodanganyika na walaghai ambao huwataka kutoa pesa ili kuwauzia mitihani kitendo ambacho huonesha kutojiamini na ni kinyume cha sheria za nchi.
“Nitoe onyo kwa walimu, wazazi na wanafunzi wawe makini na vitendo vya udanganyifu au kushiriki njama za kununua mitihani jambo hili ni batili na ni kinyume cha sheria za nchi na ikithibitika mtu amekiuka taratibu husika basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amefafanua Waitara.
Aidha Naibu waziri huyo amesema tayari Serikali imeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kufanya udanganyifu wa mitihani hiyo kwani vitendo kama hivyo vinakuwa havina tofauti na ulaji au utoaji rushwa ikiwemo na wizi.
Hata hivyo katika upande mwingine Waitara amewapongeza Wanafunzi wote na kuwatakia kila la heri ikiwemo kuwaasa wamtangulize Mungu ili akapate kufanikisha azma yao ya ufaulu na kutimiza ndoto za maisha yao ya baadaye.
“Sisi kama Serikali tunawapongeza kwa uvumilivu wao kimasomo tangu walipojiunga kidato cha kwanza mpaka sasa wanapomaliza masomo yao tunawatakia heri na wafanyie kazi yale yote waliyojifunza kwa miaka minne na wamtangilize mbele mwenyezi Mungu kwa yote,” ameongeza Waitara.
Akizungumzia mafanikio ya elimu bure ambayo ilitangazwa na Rais Magufuli na wanufaika wa kwanza kwa miaka minne wakiwa ni wahitimu wa mwaka huu Waitara amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho na kutatua changamoto zote ambazo zipo ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya kielimu kwa wanafunzi na walimu.
“Toka Rais atangaze elimu bure watahiniwa hawa wanakuwa wa kwanza kumaliza elimu yao kwa kusoma miaka minne bila malipo haya ni mafanikio makubwa na yanafanikisha lengo la serikali ya Rais Magufuli ya kumpatia mtoto elimu isiyo na mawazo ya ada na pia kupambania ufutaji wa ujinga,” amebainisha Waitara.
Kwa mujibu wa Naibu waziri huyo wa TAMISEMI amesema Serikali imekua ikitenga zaidi ya shilingi Bilioni 23 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure huku idadi ya wanafunzi wanaomaliza kwa mwaka huu wa 2019 ikiwa ni kubwa zaidi ya ile ya 2018 kwani waliosajiliwa kufanya mitihani ni 485,000 na kwa mwaka jana waliofanya mitihani ni 427,000.