Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amewataka wadau wanaotekeleza afua za malezi dhidi ya Mtoto kushirikiana na TAMISEMI hasa katika ngazi ya Halmashauri, ili kuandaa mkakati wa Ulinzi na Malezi kwa Mtoto
Mpanju ameyasema hayo hii leo Julai 13, 2023 Jijini Dodoma, wakati wa Uzinduzi wa Kitaifa wa Wadau Wanaotekeleza Afua za Malezi na Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watoto, huku akiwataka wadau hao kufanya vikao kila mwaka ili kutathimini malezi ya Mtoto.
Amesema, “mnapaswa kutengeneza afua ya kumsaidia mtoto endapo amefanyiwa ukatili na watu wa familia kuona namna itakayomsaidia kutoa taarifa kwa mtu anaemwamini hasa katika kituo cha Polisi na kila mwaka angalieni namna ya kufanya vikao mara mbili kwa ajili ya kutathimini malezi ya watoto.”
Naye Mkurugenzi kutoka Wizara hiyo, Sebastian Kitiku amesema changamoto za malezi katika jamii zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara na moja ya sababu zinazopelekea hali hiyo ni mwingiliano wa mila na desturi za jamii mbali mbali.
Hata hivyo, Mkurugenzi Huyo amewataka wazazi kupata nafasi ya kuzungumza na mtoto kila mara ili kujua kila changamoto anayopitia ili kuweza kutatuliwa kwa haraka.