Baada ya hivi karibuni Serikali kuwasilisha Bungeni muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania ya Mwaka 2018, wadau wameendelea kutoa maoni yao ambapo Kaimu Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Waalimu Tanzania, (CWT), Ezekiel Oluoch ameunga mkono muswada huo.
Amesema kuwa muswada huo utakuwa na msaada mkubwa kwa taifa kama ilivyo kwa nchi za Nigeria na Afrika Kusini ambazo ndio nchi pekee Afrika zenye Bodi ya Waalimu hivyo Tanzania itakuwa ya tatu.
”Muswada huu uko sawa kabisa na utaleta thamani kwa fani ya ualimu pamoja na ufanisi kwani kutakuwa na uwezo wa mwalimu kupokonywa leseni yake endapo atakiuka maadili ya walimu lakini zaidi ya hayo ni muhimu kwa tasnia kuwa na bodi ambayo ni kama mlezi,” amesema Oluoch ambaye pia ni mwalimu kitaaluma
Aidha, Oluoch amewataka Watanzania kutochanganya vitu ambapo wengi wamekuwa wakihusisha kuwa bodi hiyo itaongeza vyombo vinavyowasimamia walimu kitu ambacho amesema si kweli kwani bodi itahusika na kuendeleza na kusimamia taaluma ya ualimu na mwalimu mwenyewe na sio masuala ya ajira ambayo yapo chini ya utumishi na TAMISEMI.
Akiwasilisha muswada huo Bungeni Septemba 5, 2018, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, alisema walengwa katika bodi hiyo ni walimu au mtu yeyote aliyefuzu mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu au Chuo Kikuu kinachotambuliwa na mamlaka husika katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada