Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamini Mchwampaka amewataka wadau wa madini kujikita katika shughuli za ukataji na usanifu wa madini badala ya kusanifiwa nje ya nchi ili kuwezesha adhma ya Serikali ya Tanzania kuwa ya Viwanda katika Sekta ya madini.
Ameyasema hayo wakati wa kufunga maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia Mei 3-5, 2017.
Amesema kuwa, uwepo wa shughuli za ukataji na unga’rishaji wa madini hayo nchini kutawezesha kuyaongezea thamani ikiwemo kupanua wigo wa ajira kupitia sekta ya madini.
” Tanzania ya sasa ni ya Viwanda. na sisi sekta ya madini tuwe na viwanda vyetu vya kusanifu madini yetu hapa hapa nchini, kwanza tutayaongezea thamani madini yetu lakini pia tutazalisha ajira kwa wingi,” amesema Mchampaka.
Aidha, Mchwampaka ameongeza kuwa, tayari Wizara ya Nishati na Madini imewasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya biashara ya Madini nchini ili kuondoa kero ambazo ni kikwazo katika biashara hiyo kwa watanzania.
Katika mnada wa Madini ya Tanzanite jumla ya kampuni 48 zilishiriki mnada huo ambapo madini ghafi ya Tanzanite kutoka Kampuni ya TanzaniteOne yenye jumla ya gramu 691,060.33 ziliuzwa katika mnada huo kwa dola za Marekani 3,161,860, sawa na asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa kwa mauzo.
Pia, alizungumzia ujumbe wa Serikali ya Nigeria iliyoshiriki Maonesho hayo na kueleza kuwa, ujumbe huo ulifika kwa lengo la kujifunza namna Tanzania inavyoongeza thamani madini yake ikiwemo pia kubadilisha uzoefu na kuongeza kuwa, lengo ni kuifanya Afrika inufaike na rasilimali zake za madini.
Ujumbe wa Serikali ya Nigeria uliongozwa na Waziri wa Madini na Maendeleo ya Viwanda, Abubakar Bwari aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abbas Mohamed pamoja na ujumbe wa wafanyabiashara wa Madini kutoka nchini humo