Wadau wanaofanya tafiti mbalimbali za Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo ya vijijini kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo Serikalini na katika Mashirika mengine ya Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi na kusudio la tafiti hizo liweze kufikiwa.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina wakati wa Mkutano uliohusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kiuchumi uliozihusisha Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za tafiti mbalimbali na matokeo hayo huwasilishwa katika ngazi husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya jamii hasa vijijini.
“Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi ambao umejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na Mabadiliko hayo, umetokana na andiko la Wanafunzi wa Chuo hicho waliokwenda katika mafunzo kwa vitendo vijijini na kushuhudia namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri maendeleo ya wananchi”. Amesema Prof. Lokina
Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo vijijini- Dodoma, Dkt. Frank Hawassi, amezitaka Taasisi na Mashirika ya umma na Binafsi kuunganisha nguvu katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa kama juhudi hazitachukuliwa athari zake zitampata kila mmoja.
Amesema kuwa hakuna nchi inayoweza kufanikiwa kukabiliana na tatizo hilo bila kushirikiana hata kama nchi hiyo imeendelea kwa kiasi kikubwa. Pia Jamii inapaswa kujua kuwa hata matatizo ya wafugaji, wakulima na wengine kuhusu ardhi ni matokeo ya athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, hivyo kila mmoja anatakiwa kuwa chachu ya utunzaji wa mazingira, ili maendeleo yanayopatikana yawe endelevu.
Kwa upande wake aliyekuwa Balozi wa Umoja wa ulaya nchini Tanzania Tim Clarke, ambaye ameongoza timu ya washirika wa Maendeleo katika Mkutano huo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kujitahidi kuwahamasisha wananchi kutumia Nishati mbadala ikiwemo Gesi ili kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu kwa kukata miti kwa ajili ya kupata Mkaa.