Wadau wa sekta ya utalii na hoteli mkoani Tanga wametakiwa kuzingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi ikiwa ni mkakati mojawapo wa kujiandaa kunufaika na fursa mbali mbali za kiuchumi ukiwemo mradi mkubwa wa bomba la mafuta la Hoima Mkoani Tanga.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima katika ujumbe wake uliofikishwa kwa wadau hao kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja wakati akifungua kikao cha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na wadau hao.

“Nitumie fursa hii kuwaeleza kwamba nyinyi kama wadau wa sekta ya utalii na hoteli mna mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwani sekta hii inashika nafasi ya pili baada ya sekta ya uzalishaji hivyo pamoja na umuhimu huo nilioueleza nitumie nafasi hii kuwasihi kuzingatia taratibu muhimu za afya na usalama mahali pa kazi,” ameeleza mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa na kuongeza kuwa.

“Nadhani mmeshuhudia jitihada zinazofanywa na serikali ili kuinua sekta ya utalii iliyokuwa imeyumba kidogo kutokana na athari za janga la uviko-19. Jitahadi hizo zinaongozwa na Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan ambaye aliweza hata kushiriki katika filamu ya The Royal Tour yenye lengo la kutangaza vivutio vyetu vya utalii. Lakini pia amekuwa akifanya jitahadi nyingine nyingi za kuwavutia wawekezaji na hivyo kuzalisha fursa nyingi za kiuchumi ambazo endapo hatutaweza kufanya biashara zetu kwa kuzingatia sheria za nchi na viwango vya kimataifa ikiwemo masuala ya afya na usalama mahali pa kazi fursa hizi zitatupitia mbali.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Alexander Ngata, ambaye alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kikao hicho ni cha mashauriano na kuwataka washiriki kufuatilia kwa makini mada zilizoandaliwa pamoja na kueleza changamoto zinazowakumba katika utekelezaji wa masuala ya usalama na afya katika sehemu zao za kazi.

Faida ya nyanya chungu kwa wanandoa
Russia yakataa kusitisha vita Ukraine