Wadau wa utamaduni nchini wametakiwa kutumia maadhimisho ya wiki ya Utamaduni wa Washirazi kuenzi, kuendeleza na kudumisha ushirikiano wa kiutamaduni katika tasnia ya Lugha, Sanaa, Filamu, Mila na Desturi za Tanzania na Iran.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Petro Ryatuu wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Utamaduni wa Washirazi leo Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni.
“Uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Iran ulianza tangu karne ya 18 kipindi cha majilio ya wahenga wa kishirazi kutoka uajemi ulioacha turathi za kiutamaduni za pande zote mbili” amesema Ryatuu.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Watu wa Iran nchini Tanzania. Mussa Far’hanqi ameushukuru uongozi wa Tanzania kuendeleza na kuthamini utamaduni wa washirazi unaounganisha nchi ya Iran na Tanzania.
Washirazi walikuja nchini tangu karne ya 18 kufanya biashara katika Pwani ya Bahari ya Hindi na mji wao wa kwanza kufika ulikua ni Kilwa mji ambao uliweza kustawi kiuchumi na kuweza kujitengenezea fedha zake yenyewe na kufanya biashara na miji yote ya Pwani ya Afrika Mashariki.