Siku moja baada ya kuapishwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, wadau mbalimbali wamejitokeza na kutoa maoni yao kwamba wana imaní ataifikisha mbali sekta hiyo.

Rais DK. Samia Suluhu Hassan juma hili alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu ambapo alimteua Ndumbaro kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Vilevile alimuhamisha aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dk. Pindi Chana kwenda kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa michezo wamesema wana imani na Dk. Ndumbaro kwani amekaa katika sekta hiyo kwa muda mrefu.

Kocha Joseph Kanakamfumu, amesema amefurahishwa na kitendo cha Rais Dk. Samia kumteua Ndumbaro katika wizara hiyo kwani amekuwa muumini wa michezo.

Amesema hiyo ni wizara nyeti kwani imekuwa ikichangia mafanikio katika michezo mbalimbali na burudani, hivyo anaamini Ndumbaro ataitendea haki na kuhakikisha Tanzania inaendelea kupiga hatua kupitia wizara hiyo kutokana na waziri huyo kuwa mwanasheria.

“Ninampongeza Ndumbaro kwani amekuwa katika michezo hasa soka kwa kipindi kirefu sasa.

“Nina imani atatatengeneza mifumo ambayo itaendelea kuisaidia sekta hiyo kuwa biashara na wanamichezo wengi kunufaika na kazi zao na kuacha alama ikiwemo katika timu za Taifa,” amesema Kanakamfumu.

Naye mchezaji wa zamani wa Young Africans, Ramadhan Kampira alisema Ndumbaro ni mtu wa michezo hivyo nafasi hiyo inamfaa kwa kiasi kikubwa.

“Nina imani na Ndumbaro kwani ni mtu sahihi katika sekta ya michezo, amekuwa ndani ya sekta hiyo kwa kipindi kirefu na tayari alishawasaidia vijana wengi kufikia malengo na kama wachezaji wa zamani tuna imani na utendaji wake wa kazi atatufikisha mbali,” amesema Kampira.

Naye mchezaji wa zamani wa Simba, Taifa Star ambaye kwa sasa ni Kocha wa timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni, Boniface Pawasa, alisema kuwa ana imani Ndumbaro atafanya kazi vizuri na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ kwani kwa sasa ameshazoea mazingira.

“Nichukue fursa hii kumpongeza Ndumbaro kwani ameaminiwa na Rais Dk. Samia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya michezo, baada ya miaka miwili tutakuwa na maendeleo zaidi katika sekta ya michezo nchini,” amesema Pawasa.

Mbappe kukutana na uongozi PSG
Gareth Southgate afichua siri ya Sterling