Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema Tanzania ni nchi ya 14 duniani na ya 2 Afrika katika uzalishaji wa asali, huku akiwataka Wadau wa ufugaji nyuki nchini, kutumia fursa ya mkutano ujao wa Dunia wa Ufugaji Nyuki – APIMONDIA, kibiashara kwa kunadi mazao ya nyuki na utalii.
Kairuki ameyasema hayo katika mkutano wake na Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano huo kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili Barani Afrika kupewa jukumu hilo kubwa tangu kuanzishwa kwa APIMONDIA miaka 130 iliyopita.
Amesema, “tumieni mkutano huu kuongeza tija katika ufugaji na biashara ya mazao ya nyuki, kuongeza wigo wa mashirikiano na taasisi mbalimbali duniani katika kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo pamoja na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za ufugaji nyuki hususani teknolojia na mbinu mbalimbali za kuboresha na kuendeleza sekta hii.
Aidha, Kairuki pia ametoa wito kwa Watanzania na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa kwa sasa uzalishaji wa asali ni tani 32,000 pekee wakati Taifa lina uwezo wa ku¹zalisha tani 138,000.