Serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), pamoja na wadau wamezindua mfumo wa kuchunguza watoto 40,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano, kubaini iwapo wanakabiliwa na udumavu ili waweze kupatiwa huduma haraka iwezekavyo.
Taarifa ya UNICEF, iliyotolewa katika miji ya Port-au-Prince, Haiti na New York, Marekani inasema watoto watakaobainika watafikishwa katika vituo vya karibu vya afya ambako tayari huduma bora inatolewa kwa watoto 8,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano, ambao wamebainika kuwa na udumavu.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti, Bruno Maes amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema, “Tunapambana dhidi ya utapiamlo na kipindupindu, unaoweka maisha ya watoto hatarini, kipindupindu kinasambaa kwa kasi na kuna uwezekano mlipuko wa ugonjwa huu ukashindwa kudhibitiwa.”
Amesema, janga nchini Haiti kwa kiasi kikubwa limeathiri watoto kwa kuwa mgonjwa mmoja wa kipindupindu kati ya watatu ni mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano na kwa watoto ambao ni dhaifu kwa ukosefu wa lishe bora, wanaougua kipindupindu ikiwemo kuhara na kutapika, wapo karibu na kifo.