Polisi Kata ya Mbwewe, Wilayani Chalinze Mkoani Pwani, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Bruno Luambano amewataka madereva wa pikipiki (Bodaboda), kufanya kazi zilizo halali na kuacha usafirishaji wa dawa ya kulevya.
Akizungumza na bodaboda hao, Mkaguzi Msaidizi Bruno aliwaeleza kuwa wanatakiwa kuheshimu kazi yao kwa kupakia mizigo halali ikiwemo abiria na kuacha kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuwaharibia maisha.
Amesema, “kabla ya kupakia mzigo wa abiria jiridhishe kuwa umebeba nini ili kuepusha kujiingiza kwenye makosa mbalimbali ikiwemo kusafirisha madawa ya kulevya ambapo utakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Aidha, Mkaguzi Luambano pia aliwahimiza bodaboda hao kutokupakia abiria zaidi ya mmoja, kuvaa kofia ngumu, kuheshimu sheria za usalama barabarani na kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.