Wafanyabiashara wa Soko Kuu Mafinga kwa kushirikiana na serikali wameanza kukarabati barabara zilizopo ndani ya soko hilo kwa kutumia tofali za saruji ili kuondoa changamoto ya uwepo wa vumbi na matope ambayo imeonekana kuwa kero kwa muda mrefu sokoni hapo.
Wakizungumza na mtandao huu viongozi wa wafanyabishara wamesema wameamua kutumia matofali katika kufanya ujenzi huo badala ya kutumia lami kutokana kukosa fedha na kwamba kwa kuanza watajenga barabara ya urefu wa mita 150 kwa gharama ya shilingi milioni 6.
Hata hivyo wafanyabiashara hao wameeleza baadhi ya changamoto zinazowakabili sokoni hapo kuwa ni pamoja na ubovu wa barabara hizo na kusababisha vumbi katika bidhaa.
Aidha Katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika hivi karibuni, madiwani walihoji sababu za kutumia tofali kujenga barabara hizo wakihofia uimara ukilinganisha na matumizi makubwa ya barabara hizo.