Wafanyabiashara wa soko la Mkwajuni Wilaya na Mkoa wa Songwe, wametakiwa kuwa na mbinu mbadala za kulinda biashara zao ikiwemo kuajiri Walinzi Vijana na waliopitia mafunzo ya kijeshi.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi Theopista Mallya alipokutana na wafanyabiashara hao kwa ajili ya kujadili masuala ya kiusalama.
Amesema, “ushirikiano ni kitu muhimu sana mnatakiwa muongozwe na upendo katika shughuli zenu za hapa sokoni kila mfanyabiashara amlinde mwenzake kwa kuangalia duka kwa duka, genge kwa genge jambo ambalo litapelekea kupunguza uhalifu kwani mara zote udhaifu wa eneo moja unaweza kuzibwa na uimara wa eneo lingine.”
Wakiongea katika eneo hilo, Viongozi wa Soko na baadhi ya Wafanyabiashara walimpongeza Kamanda Mallya na kusema wamefurahishwa na ujio wake huku wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa taarifa za uhalifu.