Wafanyakazi kupitia Kamati ya Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) wamepinga kanuni mpya zilizobadili kikokotoo cha mafao na kutoa asilimia 25 pekee kama malipo ya mkupuo kwa mstaafu.
Kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari, TUCTA wameeleza kuwa hawakubaliani na kanuni mpya na kwamba walijaribu kuzuia kupitishwa kwa kanuni hizo katika vikao kadhaa walivyokaa na Serikali, lakini walishindwa kufanikisha azma yao baada ya kuzidiwa idadi ya kura kwenye vikao husika.
TUCTA wameeleza kuwa kanuni hizo mpya zimesababisha kushuka kwa morali ya wafanyakazi nchini hali inayozorotesha pia ufanisi wa kazi.
“Ni ukweli usiopingika kuwa, ujio wa Kanuni hizi zinazomlipa mstaafu robo ya Mafao yake (25%) kama malipo ya mkupuo na kubakiza robo tatu (75%) ambazo Serikali inadai watalipwa kama pensheni ya kila mwezi ni kanuni kandamizi ambazo zimepokelewa na wafanyakazi kwa mtazamo hasi,” imeeeleza taarifa hiyo ya TUCTA.
“Mfanyakazi akilipwa robo ya mafao yake na kubakiza robo tatu, ni wazi kuwa wengi watakaopoteza maisha kabla ya kutimiza umri wa miaka 12.5 baada ya kustaafu, wataacha fedha nyingi katika mifuko, fedha ambazo kama wangepewa kama malipo ya mkupuo zingewezesha kuinua hali za familia zao na jamii kwa ujumla. Katika hili, wafanyakazi tunasema haiwezekani na hatukubaliani nalo,” imeongeza.
Aidha, TUCTA wamedai kuwa sababu walizopewa na Serikali kuhusu uamuzi kubadili asilimia, kutoka 50% za awali hadi 25% sasa kuwa ni kutaka kuokoa mifuko ya PSPF na LAPF ili isifilisike, sababu ambazo hata hivyo walizipinga wakieleza kuwa sio za kweli. TUCTA wamedai kuwa kufilisika kwa mifuko hiyo kunatokana na malimbikizo ya deni kubwa la fedha ambazo Serikali inadaiwa na mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Taarifa hiyo ya TUCTA imekuja ikiwa ni saa chache tangu Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya kueleza kuwa atawasilisha hoja binafsi bungeni kupinga kanuni ya kikokotoo kinachotoa 25% ya malipo ya mkupuo kwa mstaafu.
Serikali imeunganisha mifuko ya Hifadhi za Jamii na kuunda mifuko miwili pekee ambayo ni NSSF na PSSSF ambayo imeundwa kutokana na EGPF, PPF, LAPF na PSPF.