Klabu ya Arsenal imetangaza kukamilisha mpango wa kuwasainisha mikataba mipya wachezaji watatu kutoka nchini Ufaransa Olivier Giroud, Laurent Koscielny na Francis Coquelin.
Arsene Wenger alisema: “Tunafuraha kuwafahamisha kwamba, tumefanikisha azma ya kuwasainisha mikataba mpya wachezaji wetu watatu, na watakua hapa kwa kipindi kingine kirefu.”
Giroud, mwenye umri wa miaka 30, alijiunga na Arsenal mwaka 2012 na amekua na msaada mkubwa kwenye kikosi cha klabu hiyo kwa kufunga mabao muhimu sambamba na kutoa pasi za mwisho zinazozaa magoli.
Hivi karibuni alifunga bao lililouteka ulimwengu wa soka (scorpion kick) walipocheza dhidi ya Crystal Palace, na alitoa pasi za mwisho ambazo zilizaa mabao mawili kati ya matatu katika mchezo dhidi ya AFC Bournemouth waliolazimishwa sare ya mabao matatu kwa matatu.
Alifunga bao la ushindi katika mchezo wa kombe la FA mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Preston, ambao walikubali kufungwa mabao mawili kwa moja.
Halikadhalika kwa mfaransa mwenzake Koscielny, amekua na mchango mkubwa katika safu ya ulinzi tangu alipojiunga na The Gunners mwaka 2010.
Kwa Coquelin, amechangia sana kuleta chachu kwenye nafasi ya kiungo tangu aliporejeshwa klabuni hapo baada ya kutolewa kwa mkopo mara kadhaa, na kwa msimu huu ameanza katika kikosi cha kwanza mara 15 katika michezo 20 ya ligi kuu ya England.