Tqkribani watu sita wamefariki huko Kihunguro, Ruiru, kaunti ya Kiambu nchini Kenya wakiwa katika tukio la harusi, baada ya kutumbukia katika kisima walichokuwa wamesimama juu yake.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Star, Polisi wamesema kundi hilo lilikuwa limefika katika makazi hayo kwa ajili ya sherehe ya harusi ambapo walikuwa wamesimama kwenye kisima hicho cha zege.
Wamesema waathiriwa sita wakiwemo watoto walifariki baada ya mfuniko wa kisima kuporomoka na kuwazamisha huku wengine 17 wakijeruhiwa.
Mtoto mmoja alifariki papo hapo huku kundi jingine likiokolewa na kukimbizwa hospitalini huku tukio hilo lilisababisha kuahirishwa kwa harusi huku polisi wakiendelea na uchunguzi.
Polisi walisema wengine watano walithibitishwa kufariki walipofika katika hospitali moja huko Ruiru, kikosi cha zima moto kutoka Kiambu kilikimbia kuokoa kundi hilo lililokuwa limenasa kwenye tanki la maji la chini ya ardhi.
“Wengi wao wameokolewa kupitia juhudi za serikali ya Kaunti ya kikosi cha zima moto cha Kiambu na wanajamii. Kazi ya uokoaji inaendelea. Tunasikitika kwa familia zilizoathiriwa na tunawatakia waathiriwa ahueni ya haraka,” amesema Wamatangi.