Wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Madagascar wameandamana kumpinga rais wa nchi hiyo pia kupinga ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya wananchi wanaoipinga serikali ambapo watu wawili waliuawa mwishoni mwa wiki.
Rais wa Madagascar, Hery Rajaonarimampianina amelaani maandamano hayo yaliyofanyika siku ya Jumapili na kuyaita mapinduzi, na kuwaonya wale aliowaita wafanya vurugu.
“Natoa wito kwa watu wote wa Madagascar kuwa watulivu, kuheshimu demokrasia, lakini kilichotokea Jumamosi si kingine bali ni mapinduzi,” amesema rais Hery
Aidha, siku ya Jumapili vikosi vya usalama vilipiga marufuku watu kuingia katika uwanja wa May 13 katikati mwa mji mkuu Antananarivo wakati wa majira ya asubuhi, kabla ya kuondoka na kuwaruhusu waandamanaji kukusanyika kwa amani.
Hata hivyo, Waandamanaji wamekuwa wakiandamana dhidi ya sheria mpya za uchaguzi, ambazo wapinzani wanadai kuwa huenda zikawazuia baadhi ya wagombea kushiriki katika uchaguzi ujao wa rais.