Jamii ya Wafugaji nchini imetakiwa kuacha tabia ya kuwatumia watoto wadogo kwa ajili ya kwenda kuchunga mifugo, hali inayopelekea ongezeka la matukio ya wizi wa mifugo kwani hawana uwezo wa kukabiliana na wahalifu pindi wanapojitokeza.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa mifugo Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Simon Pasua ameyasema hayo alipotembelea Kijiji cha Rozilini kilichopo Kata ya Enduimet Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kutoa elimu ya kuhamasisha wananchi kuhusiana namna ya kuzuia wizi wa mifugo.
Amesema, kwa kipindi cha kuanzia mwezi januari hadi machi mwaka huu jumla ya watuhumiwa 372 walikamatwa wakiwa na mifugo 3,192 ya wizi na kwamba watuhumiwa 116 kati ya waliokamatwa walifikishwa mahakamani na kupatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela vifungo mbalimbali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji hicho, John Ndikilo amewataka wafugaji wenzake kuacha kuwapeleka watoto sehemu za kuchungia mifugo kwani kitendo hicho ni kuhatarisha usalama wao pamoja na mifugo ikiwemo haki ya msingi ya kupata elimu huku Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rosilini, Luka Ngemoryo akisema kijiji hicho kinakabiliwa na ukosefu wa sehemu za malisho na kuiomba Serikali iwapatie maeneo.