Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesitisha operesheni ya kuwaondoa na kuwachomea nyumba, mazizi ya mifugo, makambi ya uvuvi ya Wananchi wa Kijiji cha Vilima vitatu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara na kuunda timu ya wataalam kutoka Wizara 8 kufuatilia utekelezaji wa operesheni hiyo na kuwasilisha ripoti hiyo serikalini kwa maamuzi zaidi.

Operesheni hiyo iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu imesababisha wananchi wengi kukosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kuchomwa moto ambapo kwasasa wanaishi chini ya miti hali iliyosababisha adha kubwa kwa wanawake wajawazito, watoto na wagonjwa.

Pia mifugo yao kuvamiwa na wanyama wakali na mingine kupotea baada ya mazizi kuchomwa moto, shughuli za uvuvi kusimama baada ya makambi na zana za uvuvi kuteketezwa kwa moto hali ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi na kushindwa kujua la kufanya.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Vilimavitatu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu huku idadi kubwa ya wananchi wakiangua vilio mbele ya Waziri Mpina wakionyesha masikitiko yao kuhusiana na unyama waliofanyiwa na Serikali ya wilaya hiyo, wamemuomba awasaidie ili waweze kurudi katika maisha yao ya awali.

Aidha, wamesema kuwa mbali na madhara hayo pia akiba ya chakula walichokuwa nacho majumbani mwao nacho kimechomwa moto hivyo kukosa kabisa chakula na kumuomba waziri huyo afikishe kilio hicho kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili wapatiwe msaada wa haraka wa chakula ili kunusuru wasife kwa njaa katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.

Kwa upande wake Waziri Mpina amesema kuwa operesheni imefanyika kinyume cha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya mwaka 2008, Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za chakula cha Mifugo namba 13 ya mwaka 2010 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003.

Pia Waziri Mpina ameitaja kasoro nyingine ni kutokamilika kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwani kama ungekamilika ungekuwa ndio mwarobaini wa migogoro katika Kijiji cha Vilima Vitatu na vijiji vingine 9 vinavyounda Hifadhi ya Wanyamapori Burunge.

Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati Vijijini, Filbert Mdachi amesema kuwa CCM imesikia malalamiko ya wananchi na amewahakikishia kuwa haki itatendeka na kumshukuru Waziri Mpina kwa kufika eneo hilo ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo uliosababisha adha kubwa kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizaberth Kitundu amekiri kuwa operesheni hiyo ilifanyika baada ya kudaiwa kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo hayo na kukiri kupokea maelekezo kutoka mkoani.

Lugola aitaka bodi ya Magereza kuhakikisha inajitosheleza kwa chakula
Mkurugenzi wilaya ya Chemba akanusha taarifa za kupigana na mtumishi wake