Serikali ya Tanzania imewataka wafugaji wenye mifugo mingi nchini kujiweka tayari kwa ajili ya kuhamia kwenye maeneo yatakayotengwa na Serikali katika ranchi mbalimbali nchini ili waweze kufuga kisasa.

Ametoa kauli hiyo Waziri mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda cha kusindika nyama cha Nguru Hills Ranch kilichoko wilayani Movomero, amewataka wafugaji kushirikiana na Serikali katika kuboresha miundombinu ya maeneo hayo ikiwemo ujenzi wa visima vya maji na majosho ili ufugaji wao uwe na tija.

Majaliwa amesema kitendo cha wafugaji hao kuhamia katika ranchi kitawezesha mifugo yao kuwa na ubora kwa sababu aina ya ufugaji wa sasa ya kutembeza mifugo umbali mrefu inasababisha ufugaji wao kuwa na tija ndogo.

Kuhusu uwepo wa kiwanda cha kuchakata nyama wilayani Mvomero Waziri Mkuu amesema kitamaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wafugaji watapata fursa ya kuuza mifugo yao kiwandani hapo.

“Uwepo wa viwanda katika maeneo yetu utatuwezesha kupunguza matatizo tuliyonayo katika maeneo yetu ikiwemo suala la migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Viwanda ndiyo vitakavyotuondoa kutoka katika uchumi wa chini hadi wa kati,” Majaliwa.

Mkurugenzi na Mshauri wa kiwanda cha Nguru Hills Ranch, Dunstan Mrutu alisema kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 300, mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku kinatarajiwa kufunguliwa mwezi Desemba mwaka huu.

Mkurugenzi huyo alisema takriban asilimia 80 ya nyama itafungashwa na kuuzwa nje ya nchi  hasa Uarabuni kwa sababu nyama ya mbuzi ya Tanzania imebainika kuwa na mvuto maalum katika nchi hizo.

“Tunatazamia pi kuwekeza katika mnyororo wa thamani kuanzia kusindika ngozi inayotoka kiwandani hadi kuzalisha viatu, mikanda na bidhaa zote za ngozi na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,”Mrutu.

Mrutu alisema nia yao ni kuitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli wa kutaka viwanda vizalishe viatu nchini kuanzia vya majeshi na wananchi wote ambapo wamepanga kuanzia mwakani wataanza kuuza bidhaa hizo.

Pia amesema kuwa uwepo wa kiwanda hicho utatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kuuza majani, mifugo na mazao ya chakula kama mtama, mahindi, ambapo tayari wameanza kuhamasisha jamii za wafugaji na wakulima wa Mvomero, Ngerengere na sehemu zinazozunguka eneo la kiwanda kuchangamkia fursa hiyo.

 

Dhamira Ya Kipre Tchetche Yatimia
Jose Mourinho: Bado Usajili Wa Mchezaji Mmoja