Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Massauni amemuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini kuwasimamisha kazi Askari wanne wa Jeshi la Magereza katika Gereza kuu la Ruanda Mbeya baada ya kubaini wafungwa wa gereza hilo kumiliki simu na kutumia madawa ya kulevya wakiwa gerezani.
Ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Gereza hilo na kuzungumza na wafungwa pamoja na kufanya ukaguzi ulioonesha kuwa simu hizo zinatumika kwa kufanya vitendo vya rushwa kwa kutumiana miamala ya kifedha baina ya wafungwa au ndugu wa wafungwa na askari hao.
Aidha, kufuatia ukiukwaji huo wa taratibu, Naibu Waziri Masauni amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini kuwasimamisha kazi Askari wanne ambao wamebainika kutumia simu hizo za wafungwa kupitia miamala ya kifedha ambayo imeonekana baada ya simu hizo kuchunguzwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema pamoja na hatua ambazo zimechukuliwa na Naibu Waziri Masauni, bado ipo haja ya Mkuu wa Gereza la Ruanda kujitathmini kama bado anastahili kuendelea na nyadhifa hiyo.