Waganga wa tiba asili zaidi ya 300, Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, wamekubali kusajili nyara za Serikali wanazomiliki kama sehemu ya vitendea kazi vyao ikiwemo ngozi mbalimbali za Wanyama.
Lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya kazi zao kwa kufuata taratibu za nchi kadri zinavyoelekeza, na kuwabaini wale wachache wasiotaka kufuata maelekezo ya Serikali katika utendaji wao wa kazi.
Hatua hiyo imekuja, baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga kutoa mwezi mmoja kwa waganga hao kuhakikisha kuwa wanasajili nyara za Serikali wanazomiliki ili kuwaondoa waganga matapeli.
Aidha waganga wamelipokea agizo hilo la Mkuu wa Wilaya hiyo, na kwamba njia hiyo itaondoa usumbufu wa wao kukamatwa mara kwa mara na jeshi la polisi.
Festo Kiswaga amewataka watalaam wa Serikali kuwapa maelekezo waganga namna ya kusajili vitendea kazi vyao na kuwataka wagaga hao kuwa na orodha na vitendea kazi vyao hasa vile vinavyotambulika na Serikali.