Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.

Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati wa mkutano uliofanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na kuwajulisha wananchi kilichotokea.

Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu uliopo katika mkoa.

“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni nani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe hapa kote, operesheni ipite ya kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,” Amesema Wangabo

Aidha, Mmoja wa wananchi, Debora Maenge amesema kuwa amesikitishwa sana na tukio lililotokea katika eneo hilo kwani walikuwa wakijua kwamba wanaishi na mtu ambaye ni mwema kumbe ni mtu ambaye hafai na hana ubinadamu hata kidogo.

Hata hivyo, watuhumiwa, James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake, Michael Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo kufungwa.

CUF yajikabidhi mikononi mwa CCM,'Huwezi kumdharau kiongozi wa CCM'
Wanamgambo wa Al-Shabaab wafanya mauaji