Mchakato wa kuwania nafasi za kugombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaoendelea umeibua tafrani katika jiji la Arusha ambapo wagombea wamejikuta wakirushiana ngumi.

Taarifa kutoka jijini humo zinaeleza kuwa ugomvi huo uliibuka baada ya mgombea wa mmoja anaejulikana kwa jina la Victor Njau ambaye ni mwanasheria, kuanza kutoa sera zake mbele ya wanachama wa CCM wa jimbo la Arusha Mjini na kuahidi kuwa endapo atapewa ridhaa atahakikisha anavunja ukuta/uzio katika eneo la reli linalomilikiwa na ‘mafisadi’ kinyume cha sheria, na kulirudisha mikononi mwa Shirika la Reli Tanzania.

Eneo hilo la reli linamilikiwa na mgombea mwenzake, Philemon Mollel kupitia kampuni yake ya Monaban. Kampuni hiyo imezungusha uzio mkubwa katika eneo hilo na kuendesha biashara ya kuoshea magari.

Hivyo, kauli ya Njau ilionekana kumlenga moja kwa moja bwana Mollel ambaye alishindwa kuvumilia na akaanza kujibu mapigo baada ya  kupewa nafasi azungumze na wana CCM.

Mbali na kukanusha tuhuma za kuwa fisadi zilizotolewa na Njau, Mollel alimshambulia kwa kejeli akiwaomba wapiga kura wasimchague mgombea huyo kwa kuwa amezoea kuishi maisha ya chumba kimoja, maisha ya kiholela na kwamba maisha yake ni hohehahe.

Aliongeza kuwa mbali na kuishi chumba kimoja, watu wa aina ya Njau ni watu wa kubwabwaja na kusema hovyo.

Baada ya kurushiana vijembe hivyo, wagombea hao walirejea katika ofisi za wilaya za CCM kwa ajili ya kupata utaratibu ambapo viongozi wa chama hicho waliwaonya kwa lugha walizotumia.

Hata hivyo, wagombea hao walianzisha tena majibishano makali ya maneno na kutoleana kashfa. Ghafla, Njau alimrukia Mollel na kumshambulia kwa ngumi na ugomvi wao ukaamuliwa na mashuhuda.

Baada ya tukio hilo, Mollel aliwaambia waandishi wa habari kuwa atapeleka malalamiko yake kwenye uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya kwa kuwa bwana Njau amekuwa akimfuata bila sababu za msingi kwa muda mrefu.

Kwa upande wa  bwana Njau, yeye alipoulizwa sababu za kumshambulia mgombea mwenzie alijibu kuwa Mollel aliumizwa na ukweli aliomwambia. “Ukweli huwa unauma,” alisema Njau.

Wamarekani Washambuliwa Kwa Risasi Katika Ukumbi Wa Sinema
Wenger Awaahidi Makubwa Mashabiki Wa Arsenal