Jumla ya wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku sita inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya mjini Mumbai nchini India.
Wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting) na kubadili milango miwili hadi mitatu ya moyo (Valve Replacement).
Aidha, wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na wanne kati yao wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Hata hivyo, katika kambi hiyo iliyoanza tarehe 18 hadi tarehe 23 mwezi huu inaenda sambamba na utoaji wa elimu pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa madaktari pamoja na wauguzi, ambapo Jumla ya wagonjwa 20 ambao ni watu wazima wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.